Katika siku za hivi karibuni, mashabiki wa Simba walikuwa na wasiwasi baada ya taarifa za kuumia kwa mlinda mlango namba moja wa timu hiyo, Ayoub Lakred, ambaye anatarajiwa kukaa nje ya uwanja kwa angalau wiki sita. Hata hivyo, kipa mwingine wa Simba, Hussein Abel, amewatuliza mashabiki kwa kusema kuwa kipa yeyote ana uwezo wa kuanza kwenye mchezo.
Abel, ambaye alijiunga na Simba msimu uliopita akitokea KMC, amewapongeza makocha wapya wa timu hiyo kwa uwezo wao mkubwa na jinsi wanavyowaelekeza wachezaji badala ya kuwafokea wanapokosea. Alisema kwa sasa hakuna haja ya kuwa na hofu mchezaji mmoja anapokosekana kwa kuwa kila mchezaji ana uwezo mkubwa wa kuanza kikosi cha kwanza.
“Mashabiki wasiwe na hofu, hata kama mchezaji fulani atakuwa hayupo, bado mchezaji mwingine ana uwezo wa kufanya vizuri akipata nafasi,” alisema Abel na kuongeza, “Msimu huu nimefurahi wachezaji wengi waliosajiliwa ni vijana kwa hiyo wapinzani wajipange, wachezaji wamekuja na morali nao wanataka umaarufu, wana hamu ya kutwaa makombe, wana njaa ya mafanikio, hivyo watu wajipange kweli.”
Kipa huyo ambaye kwa sasa yupo na kikosi cha timu hiyo nchini Misri, alizungumzia benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Faldu Davids akisema wana ufundishaji wa aina ya pekee unaopendwa sana na wachezaji wengi kwani ni rahisi kuwaelewa. “Walimu wetu wanajua kufundisha, wanakupa moyo, unapokosea hawakufokei, wanakuelekeza ili usirudie tena kosa ulilofanya. Halafu watu wasichokijua kocha wetu ni kocha mchezaji, yeye mwenyewe anaingia ndani anacheza na kuelekeza, hana mambo mengi, tunajivunia kuwa naye na tunaomba Mungu abaki kwa muda mrefu kuendelea kuifundisha Simba,” alisema kipa huyo.
Abel alisema kwa msimu mmoja aliojiunga na Simba amejifunza mambo mengi ambayo awali alikuwa hayajui, hivyo kwake ni somo kubwa. “Nilijisikia faraja kuingia Simba, nilikaa na wachezaji wakubwa wenye uzoefu kama Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ambao wamenipa ujasiri mkubwa ingawa haukuwa msimu mzuri kwetu. Hata hivyo, sijacheza mechi za kimataifa lakini kuwa tu kwenye timu ambayo inacheza mechi hizo nimejifunza vitu vingi ambavyo nilikuwa sivifahamu kabla. Kusema kweli ukicheza hizi timu kubwa ni shule tosha,” alisema Abel.
Akiizungumzia idara ya makipa, Abel aliwahakikishia wanachama na mashabiki wa Simba kutokuwa na wasiwasi kwani mafunzo wanayoyapata ni ya hali ya juu na bora pia.