Kibu Denis arejea kambini Simba
Baada ya kutoonekana katika maandalizi ya msimu mpya wa 2024/25, winga wa Timu ya Taifa ya Tanzania na Klabu ya Simba, Kibu Denis Prosper, amerudi rasmi kambini. Awali, iliripotiwa kwamba Kibu alikwenda kufanya majaribio nchini Norway na timu ya Kristiansund BK inayoshiriki Ligi Kuu ya huko.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amethibitisha kuwa Kibu amemalizana na kocha mpya wa timu hiyo, Fadlu Davids, na ameanza mazoezi na wenzake katika uwanja wa MO Simba Arena Bunju, Dar es Salaam.
Ahmed Ally amesema Kibu ni mchezaji wao muhimu, na ingawa alikosea kwa kutofuata taratibu alipoondoka, wamemruhusu kurejea na kuanza mazoezi. Taratibu za kinidhamu zitaendelea kufuatwa lakini jambo kuu ni kwamba Kibu amerudi kambini na ameanza mazoezi na timu yake.