Khalid Aucho amemzungumzia Duke Abuya na Mudathir Yahya, akieleza tofauti zao uwanjani na kutoa ushauri wa kiufundi.
Khalid Aucho Amchambua Duke Abuya na Mudathir Yahya Kambini Yanga
Kiungo wa Yanga, Khalid Aucho, maarufu kama Daktari wa Soka, amefunguka kuhusu uchezaji wa wenzake Duke Abuya na Mudathir Yahya. Akiwa kwenye mahojiano ya moja kwa moja kupitia insta story na mwandishi wa habari kutoka Kenya, @bedjosessien, Aucho aliweka wazi tofauti za kiufundi kati ya wachezaji hao wawili wa Yanga.
Tofauti ya Uchezaji Kati ya Mudathir Yahya na Duke Abuya
Aucho alieleza kwamba ingawa hawezi kusema ni nani bora kati yao, kuna tofauti za wazi katika mitindo yao ya uchezaji. “Wote ni wazuri wakiwa na mpira, lakini Duke anachukua muda mrefu zaidi kufanya maamuzi ya nini cha kufanya. Mudathir ni ‘aggressive’ zaidi na anapenda kupambana na kuwania mpira kwa nguvu kuliko Abuya,” alisema Aucho.
Ushauri wa Aucho kwa Duke Abuya
Aucho alikumbuka wakati Abuya alipofika Yanga kwa mara ya kwanza, na hakujua nafasi sahihi ya mchezaji huyo. “Nilipomuona kwa mara ya kwanza, sikujua anacheza nafasi gani. Alionekana kupenda kushambulia zaidi na mara nyingi alionekana kama winga. Nilimwambia, kama unataka kucheza mpira vizuri, hakikisha unajua nafasi yako. Kama wewe ni beki, cheza kama beki na si kama straika au nafasi nyingine,” aliongeza Aucho.
Msimamo wa Aucho na Tathmini ya Kikosi
Aucho alimalizia kwa kusema kuwa Yanga ina kikosi bora, na kila mchezaji anajitahidi kufanya vizuri kwenye nafasi yake. Ushauri na uchambuzi wa Aucho unaonyesha umuhimu wa kujua nafasi sahihi na kutimiza wajibu kwa ufanisi ili kusaidia timu kupata matokeo mazuri.
Khalid Aucho ameendelea kuwa msaada mkubwa kwa kikosi cha Yanga siyo tu kwa uchezaji wake uwanjani bali pia kwa ushauri wake kwa wachezaji wenzake, jambo linaloimarisha uimara wa timu.
Leave a Comment