Mgogoro wa Yusuph Kagoma na Yanga wazidi kushika kasi; nyaraka muhimu zasema yote na Yanga wametoa masharti ya kumaliza suala hilo.
Mgogoro Kati ya Yusuph Kagoma na Yanga
Yanga SC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, wamewasilisha nyaraka muhimu katika shauri linaloendelea la mkataba kati yao na mchezaji Yusuph Kagoma mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji TFF.
Makubaliano ya Mauzo Kati ya Yanga na Fountain Gate
Kabla ya kuzungumza na mchezaji, Yanga SC ilianza mawasiliano na Fountain Gate Academy (FGA) kutaka kujua uwezekano wa kumpata Kagoma. Fountain Gate waliruhusu mazungumzo kufanyika, na tarehe 27 Machi 2024, pande zote zilisaini makubaliano rasmi ya mauzo (Sales Agreement). Kwa upande wa Yanga, Mkataba ulisainiwa na CEO Andre Mtine, na kwa Fountain Gate, CEO Thabita ndiye aliyesaini.
Usajili wa Yusuph Kagoma na Nyaraka Muhimu
Baada ya makubaliano hayo, Yanga walifanya mazungumzo na Kagoma na kumleta Dar es Salaam kutoka Kigoma, ambapo alisaini mkataba wa kujiunga na Yanga mnamo tarehe 28 Machi 2024 mbele ya mwanasheria wake. Hii ilikuwa hatua rasmi ya kumalizana na FGA, ambapo pia kulikuwa na nyaraka za usajili wa Nickson Kibabage.
Nyaraka zote za mchakato huu zimewasilishwa mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji TFF, kuthibitisha kuwa Yanga walifuata taratibu sahihi katika usajili wa Kagoma.
Soma: Yanga vs CBE Sept 14: Gamondi Apanga Ushindi Mapema
Kagoma Kughairi Kucheza Yanga
Sakata lilianza pale Kagoma alipokataa kucheza Yanga, licha ya kusaini mkataba. Awali, ilidaiwa kuwa hakuwa amelipwa fedha zake kwa wakati, lakini Yanga walikuwa ndani ya makubaliano kwani mkataba unasema malipo yalitakiwa kufanyika ifikapo Julai Mosi, 2024. Sababu nyingine iliyotajwa ni kwamba Kagoma haoni nafasi yake ndani ya timu.
Yanga Watoa Masharti kwa Kagoma
Kutokana na mwenendo wa Kagoma, Yanga waliamua kumpa masharti mawili: aombe msamaha hadharani au alipe fidia ya kuvunja mkataba. Kwa upande wao, Yanga hawako tayari kumruhusu Kagoma aondoke bila kuzingatia masharti hayo, wakisisitiza kuwa nyaraka za mkataba ziko wazi na wana haki ya kuweka pingamizi.
Uamuzi wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeagiza TFF na Bodi ya Ligi kumtaka Simba SC kusitisha mara moja kumtumia Kagoma kutokana na pingamizi la Yanga. Pia, Yanga wamesema wako tayari kumsamehe Kagoma endapo ataomba msamaha hadharani, na wakiondoa pingamizi, basi mchakato utaendelea.
Kwa sasa, shauri hili bado linaendelea, na hatma ya Kagoma iko mikononi mwake na Yanga wanasubiri kuona kama atakubali masharti yao.
Leave a Comment