Haji Manara amemsilimisha rasmi Hamisa Mobetto kuwa shabiki wa Yanga
Katika tamasha la kilele cha ‘Wiki ya Mwananchi,’ Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara ‘Bugatti’ alimsilimisha rasmi Mwanamitindo maarufu nchini, Hamisa Mobetto kuwa shabiki wa timu hiyo ya Jangwani. Tukio hilo lilifanyika wakati Mobetto alipovishwa jezi ya Yanga na Stephane Aziz Ki aliyeitwa jukwaani na Manara.
Haji Manara alisema kuwa amemsilimisha rasmi Hamisa na kumvalisha jezi ya Yanga, huku msanii huyo akionekana mwenye furaha tele. Ukaribu wa Mobetto na mchezaji wa Yanga, Stephane Aziz Ki, ambaye mara kwa mara ameonekana naye katika matukio mbalimbali, ulichangia kwa kiasi kikubwa katika uamuzi huo.
Hamisa Mobetto, anayejulikana kuwa shabiki mkubwa wa Simba, alivaa jezi hiyo ya Yanga lakini hakutoa tamko lolote kuthibitisha kama ameachana na Simba na kujiunga na Yanga. Hapo awali, Mobetto alinukuliwa na Mwanaspoti akisema yupo karibu na Aziz Ki lakini bado ni shabiki wa Simba. Hata hivyo, tukio hilo limeondoa utata mbele ya mashabiki wa klabu hiyo.
Katika tamasha hilo, lililofanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, mashabiki walishuhudia tukio hilo ambalo limeacha maswali mengi kwa mashabiki wa Simba na Yanga. Je, Hamisa Mobetto sasa ni shabiki wa kudumu wa Yanga? Wakati utasema.
Leave a Comment