Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema haoni umuhimu mkubwa wa kuwafahamu wachezaji wapya wa Simba SC, bali ameweka mkazo katika maandalizi ya timu yake kwa ajili ya mchezo wa kesho.
Akizungumza na wanahabari leo kuelekea mechi ya Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mkapa saa 1:00 usiku, Gamondi alisema, “Ninawaheshimu sana wapinzani wangu wote, hakuna underdog kati ya Simba na Yanga. Simba wana kocha mpya na wachezaji wapya wanaotaka kumuonesha uwezo wao, hivyo watakuwa na ari kubwa kama sisi.”
“Mchezo huu utakuwa ni wa uwiano wa 50/50 mwanzoni, kushinda haimaanishi kwamba uko bora zaidi, lakini ni muhimu kuhakikisha tunakuwa bora msimu mzima kwa mafanikio ya klabu yetu bila kujali mpinzani ni nani.”
“Tunawaandaa wachezaji uwanjani na inapofika siku ya mechi, ni jukumu lao kutekeleza maelekezo yetu. Najua Simba wanacheza vizuri, itakuwa ni mechi ya kushambuliana kwa zamu na ni mchezo mgumu.”
“Sina uhakika nini kitatokea, lakini lengo langu ni kumiliki mpira na kutengeneza nafasi za kufunga. Mechi iliyopita tulitengeneza nafasi nyingi lakini hatukutumia vema, wiki hii tumefanyia kazi hilo kuhakikisha tunatumia nafasi vizuri na kurekebisha makosa kwenye ulinzi,” alimalizia Gamondi.
Leave a Comment