Timu ya Simba kwa msimu ujao wa 2024-2025 imeonekana kumshangaza Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, ambaye amekiri kwamba wapinzani wao wameimarika kwa kufanya usajili mzuri. Gamondi amesema hayo baada ya kushuhudia Simba ikishinda mabao 2-0 dhidi ya APR ya Rwanda kwenye Tamasha la Simba Day, huku Yanga nayo ikishinda 2-1 dhidi ya Red Arrows ya Zambia kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi. Mechi hizo zilichezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga na Simba zinatarajiwa kukutana Agosti 8, 2024, kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii kuelekea msimu mpya wa 2024-2025.
“Sasa tunaanza hesabu mpya kwa ajili ya mchezo wa dabi. Niliona Simba wamefanya usajili mzuri na wana timu imara. Nawakumbusha wachezaji wetu waachane na picha ya msimu uliopita,” alisema Gamondi.
Gamondi, aliyewaongoza Yanga kushinda mabao 7-2 dhidi ya Simba msimu uliopita kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara, amesema dabi ya Agosti 8 ni muhimu kwa kutoa taswira ya msimu mpya wa Yanga.
“Mchezo huu utakuwa mgumu na utatoa picha ya jinsi tunavyoanza msimu huu. Tunakutana na kikosi ambacho hakikufanikiwa kutushinda msimu uliopita, watakuja kwa nguvu mpya,” alibainisha Gamondi.
Kocha huyo wa Argentina anakumbuka walivyofungwa na Simba katika fainali ya Ngao ya Jamii msimu uliopita na safari hii anataka kubadilisha matokeo.
“Tunahitaji kuingia uwanjani kwa lengo la kubadilisha matokeo. Timu yetu itapangwa kulingana na uwezo wa wachezaji waliopo, sio majina. Tunahitaji wachezaji wenye uwezo wa kufanikisha malengo yetu,” alisema Gamondi.
Akizungumzia mechi yao dhidi ya Red Arrows, Gamondi alisema: “Mchezo ulikuwa maalum kwa kuwafurahisha mashabiki wetu kwenye siku yao kubwa.”
Hata hivyo, Gamondi aliongeza kuwa furaha ya mechi hiyo sasa imepita na wanahitaji kuanza maandalizi kwa ajili ya dabi dhidi ya Simba.
Wakati Yanga na Simba wakicheza nusu fainali ya pili ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Benjamin Mkapa, Coastal Union itapambana na JKU kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Simba ni mabingwa watetezi wa Ngao ya Jamii baada ya msimu uliopita kuichapa Yanga kwa penalti 3-1 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, baada ya sare ya 0-0 ndani ya muda wa kawaida.