Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kuwa lengo la kucheza mechi za kirafiki za ndani ni kujenga muunganiko bora wa timu na kutoa nafasi kwa kila mchezaji kuonyesha uwezo wake katika maandalizi ya kambi ya wiki mbili nchini Misri.
Amesisitiza kuwa mechi hizo zilikuwa za kiufundi na mbinu, lengo likiwa ni kuandaa timu bila presha yoyote. Hii iliwapa nafasi ya kuandaa kikosi bila mashabiki kuona kikosi chao kipya cha msimu huu.
Simba ilikamilisha maandalizi ya wiki mbili kwa msimu wa 2024/25 na kucheza michezo mitatu ya kirafiki. Jana walimaliza programu yao kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Adalah ya Saudi Arabia, mabao yaliyofungwa na Joshua Mutale na Steven Mukwala.
Kocha Davids amesema kuwa amepata muda mzuri wa kuandaa timu kwa mechi za kirafiki ambazo zimeongeza ubora wa kikosi na muunganiko wa mchezaji mmoja mmoja. Alieleza kuwa, “Zilikuwa wiki tatu nzuri za maandalizi, tumecheza mechi tatu za kirafiki, lengo likiwa si ushindi bali kuwapa nafasi wachezaji wote kucheza na kuona matokeo ya mazoezi.”
Ameongeza kuwa mechi hizo zimempa mwanga kuhusu ubora na madhaifu ya kikosi chake. “Sina mashaka kwa sababu nimeona sehemu ya ulinzi iko vizuri, kiungo na washambuliaji wanatekeleza maelekezo ya mazoezi,” amesema Davids.
Pia, alibainisha kuwa japokuwa timu imetengeneza nafasi nyingi za ushambuliaji, bado kuna haja ya kuboresha eneo hilo. “Eneo la ushambuliaji tunahitaji kuliboresha zaidi, lakini kwa ujumla timu ipo vizuri,” amesema Fadlu.
Kocha huyo ameelezea furaha yake kwa kujituma kwa wachezaji wake kila wanapopata nafasi. Alitoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi kwenye Simba Day ‘Ubaya Ubwela’ ili kuona timu yao mpya na maandalizi yao kwa msimu ujao.
Kikosi cha Simba kinarejea kesho kutoka Misri baada ya kambi yao, tayari kwa mchezo dhidi ya APR FC ya Rwanda katika kilele cha Simba Day utakaofanyika Agosti 3, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Leave a Comment