HomeMichezoElie Mpanzu Afunguka Kuhusu Simba na Safari ya Genk

Elie Mpanzu Afunguka Kuhusu Simba na Safari ya Genk

Elie Mpanzu Afunguka Kuhusu Kujiunga na Simba

Klabu ya Simba imejaribu mara tatu kuinasa saini ya Winga wa AS Vita, Elie Mpanzu, lakini mambo bado yanaonekana kuwa magumu baada ya mchezaji huyo kufunguka na kueleza kila kitu. Simba inahitaji sana huduma za Mpanzu, lakini dau la Dola 250,000 (zaidi ya Sh 500 milioni) liliwekwa na klabu hiyo ya AS Vita limewazuia Msimbazi kumnasa mapema kama walivyofanya kwa wachezaji wengine waliopo kambini Misri.

Simba ilimuona Mpanzu kama mbadala sahihi wa Kibu ikiwa atapata timu nje, kutokana na aina yao ya uchezaji wenye kasi, nguvu, na kutochoka haraka uwanjani pamoja na uwezo wa kukaba. Kwa mujibu wa Gazeti la Mwanaspoti, Mpanzu mwenyewe amefunguka ukweli kuhusu kufuatwa na Simba na kuweka bayana msimamo wake, akiitaja klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji aliyowahi kuitumikia Mbwana Samatta.

Mpanzu alisema ni kweli Simba ilikuwa ikimtaka na ilikuwa ikifanya mazungumzo na mabosi wa AS Vita, lakini msimamo wake ni kwenda kucheza soka Ulaya na sio Msimbazi. Alifichua sababu hasa ya msimamo huo wa kuikacha Simba na kutaka kwenda Ubelgiji kukipiga Genk kuwa ni familia yake pamoja na ndoto zake za muda mrefu za kucheza Ulaya.

“Familia ilinishauri kuishi katika ndoto zangu na sio kuangalia maslahi kila wakati, hiyo tu imekuwa sababu yenye nguvu sana moyoni mwangu, kwani nataka kufanya kazi kwa furaha,” alisema Mpanzu na kuongeza; “Nilitaka kuja Simba kwani nayo ni timu kubwa na nzuri, lakini kuna wakati nilitakiwa kufikiria mbele zaidi kwani hata kama ningekuja huko bado ningekuwa naiwaza ndoto yangu ya kuchezea Ulaya.”

Simba ilikuwa tayari imeshakubaliana na Mpanzu kusaini mkataba wa miaka miwili, lakini baadaye vigogo wanaommiliki winga huyo, akiwemo Rais wa AS Vita Amadou Diaby, aliingilia kati dili hilo na kumzuia staa huyo kusaini kwa kutaka dau nono zaidi, na ndilo lililowarudisha nyuma vigogo wa Msimbazi.

Kutokuja kwa Mpanzu ndani ya Simba kumewapa nafasi Willy Onana na Freddy Koublan kusalia Msimbazi, kwani awali mmoja ilikuwa lazima ampishe Mkongomani huyo, huku ikielezwa Onana alikuwa na nafasi kubwa kwa vile kuna ofa kutoka Qatar.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Latest Posts