Michezo

Dili la Mpanzu na Simba lafikia Hatua Mpya

Dili la Mpanzu na Simba lafikia Hatua Mpya

Meneja wa idara ya habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameelezea juhudi za klabu hiyo katika kumsajili kiungo mshambuliaji wa AS Vita ya DR Congo, Elie Mpanzu, zikionyesha mafanikio. Ally amethibitisha kuwa Simba wamerejea tena kwa nguvu zaidi kwa lengo la kunasa saini ya Mpanzu, ambaye alikuwa chaguo lao la kwanza katika usajili.

Ally amesema kuwa ugumu wa majadiliano ya awali ulisababisha kuchelewesha mchakato huo, lakini sasa wanafanya juhudi za ziada kuhakikisha wanamleta nyota huyo wa AS Vita. Imefahamika kuwa Simba walikuwa wamepeleka ofa ya dola 200,000 sawa na milioni 540, lakini klabu ya AS Vita ilikuwa ikihitaji dola 250,000. Kwa sasa, Simba wameongeza dau lao na kufikia dola 225,000, sawa na milioni 607.

Huku Simba wakisubiri majibu kutoka AS Vita, Mpanzu hajaungana na timu yake ambayo tayari imeanza maandalizi ya msimu mpya, na inadaiwa kuwa amepokea mwaliko wa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji. Ally amefafanua kuwa walikuwa wameacha mazungumzo kwa muda, lakini sasa wamerudi tena na wanaendelea kufuatilia kwa karibu suala hilo.

Viongozi wa Simba wanajitahidi kuhakikisha wanafanikiwa kumpata kiungo mshambuliaji huyo ili kuimarisha safu ya ushambuliaji kwa msimu ujao. “Kweli Mpanzu ni mchezaji mzuri, suala lake liko 50 kwa 50, linaenda na kurudi. Awali tulifatilia ikawa ngumu na sasa tumerejea kuona kama tutaweza kupata huduma yake,” alisema Ahmed Ally.

Kwa upande wa kumfatilia Mpanzu kama mbadala wa mshambuliaji wao Kibe Denis, Ahmed amesema kuwa suala la Denis lipo mikononi mwa mwanasheria wa Simba, wakisubiri barua kutoka klabu ya Kristiansund BK ya Norway.

Ikiwa dili la Mpanzu litafanikiwa, baadhi ya wachezaji wa kigeni wa Simba watalazimika kupewa ‘THANK YOU’, huku ikidaiwa kuwa Fredy Michael ni miongoni mwao.

Leave a Comment