Simba SC Yakamilisha Mkataba Mkubwa na Diadora kwa Utengenezaji wa Jezi
Ushirikiano wa Kihistoria Katika Sekta ya Michezo
Kampuni ya kimataifa ya vifaa vya michezo, Diadora kutoka Italia, sasa ndio itakayobuni na kutengeneza jezi pamoja na bidhaa nyingine za Simba SC kwa kipindi cha miaka mitano. Hili linafuatia makubaliano yaliyofikiwa kupitia kampuni ya Jayrutty Investment.
Jayrutty Investment imepatiwa haki ya kipekee ya kutumia nembo ya Simba kuzalisha bidhaa hizo kwa mkataba wa thamani ya Sh38 bilioni, unaotarajiwa kudumu kwa miaka mitano.
Furaha ya Simba SC Kwa Ushirikiano Mpya
Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, amesema kuwa kuona jezi na bidhaa za Simba zikizalishwa na Diadora ni hatua kubwa na heshima kwa klabu.
“Diadora ni chapa kubwa duniani, waliwahi kuvaliwa na timu ya taifa ya Italia wakati iliposhinda Kombe la Dunia, pia AS Roma na timu nyingine kubwa duniani,” alisema Mangungu.
“Simba Sports Club inazidi kukua na kuwa chapa ya kimataifa, hivyo ni lazima tushirikiane na brand kubwa kama Diadora kuonesha ukubwa wetu,” aliongeza.
Serikali Yapongeza Utekelezaji wa Mkataba
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, alishiriki kushuhudia utekelezaji wa mkataba huo.
Mwinjuma alisema amefurahishwa na namna Simba na Jayrutty Investment walivyotekeleza makubaliano yao kwa vitendo.
“Nilitaka kujua ile brand kubwa mliyosema wakati wa kusaini mkataba, na sasa nimeridhika – kweli Diadora ni brand kubwa duniani,” alisema Mwana FA kwa furaha.