Kila Kombe ni Lazima kwa Yanga, Asema Chama
Kiungo mahiri wa Yanga, Clatous Chama, amesisitiza kuwa kila kombe ni la maana kwao msimu huu, na amewataka mashabiki wa timu hiyo maarufu kama ‘Wananchi’ kujiandaa kwa burudani tele kutoka kwa wachezaji wao.
Chama alitoa kauli hiyo baada ya Yanga kutwaa ubingwa wa michuano ya Toyota Cup kwa kuwafunga wenyeji Kaizer Chiefs mabao 4-0 katika mechi iliyochezwa nchini Afrika Kusini jana, Jumapili, Julai 28, 2024.
“Mchezo ulikuwa na ushindani mkubwa, lakini tulianza vizuri kwa kufunga, hali ambayo ilirahisisha mechi kidogo. Hapa hali ya hewa ni baridi sana ikilinganishwa na Dar es Salaam, lakini tunapoingia uwanjani na kuanza kukimbia, damu inapata joto kidogo.
“Tunapoelekea kilele cha Wiki ya Mwananchi, napenda kuwashukuru mashabiki kwa sapoti yao na maombi yao. Ninahisi siku ya Mwananchi Day itakuwa siku nzuri, na ninawaalika wote tufike kusherehekea pamoja.
“Kila kombe ni muhimu kwetu sisi, na baada ya kushinda hiki, tunaongezeka nguvu na morali kama wachezaji, na mashabiki watakuwa na furaha zaidi. Tuombe msimu uwe mzuri,” alisema Chama.
Leave a Comment