Michezo

Chama Aitishia Simba: Yanga Kubeba Makombe Yote

Chama Aitishia Simba

Nyota wa Lusaka, Clatous Chama, ameonyesha furaha yake baada ya Yanga kutwaa Kombe la Toyota na kujipatia medali muda mfupi baada ya kujiunga nayo kutoka Simba. Chama amesisitiza kuwa yeye na wachezaji wenzake wanataka kuchukua kila kombe na taji lililo mbele yao kwa ajili ya mashabiki wao.

Clatous Chama Aitishia Simba sc

Akizungumza juzi nchini Afrika Kusini baada ya mchezo maalum ulioandaliwa na Klabu ya Kaizer Chiefs, Chama alisema kuwa kombe walilopata limewapa motisha ya kushinda taji lingine lililopo mbele yao.

Agosti 8, mwaka huu, Yanga itakutana na Simba katika mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Katika mechi ya juzi kwenye Uwanja wa Bloemfontein, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kaizer Chiefs, mabao yakifungwa na Stephane Aziz Ki, Prince Dube, na Clement Mzize.

“Mchezo ulikuwa mgumu lakini baada ya kufunga mabao mawili ya haraka, mechi ikawa rahisi. Lengo letu ni kushinda kila kombe na taji kwa ajili ya heshima na faraja ya mashabiki wetu ambao wamekuwa wakitupa sapoti. Nawaahidi Kilele cha Wiki ya Mwananchi watafurahi sana, waje kwa wingi uwanjani,” alisema Chama.

Beki wa kati, Dickson Job, alisema kuwa kikosi chao msimu huu kimeongeza wachezaji wenye uwezo mkubwa, na hivyo wana kikosi kipana na bora kuliko msimu uliopita. “Mchezo ulikuwa mgumu, bado hatujawa vizuri sana kwa sababu huu ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mpya. Tumeweza kutumia makosa yao kupata ushindi. Naamini kwa mechi hizi tatu tumeshaanza kupata muunganiko kati yetu na wachezaji wapya. Msimu ujao tutafanya vizuri zaidi kwa sababu tuna kikosi kipana chenye wachezaji bora,” alisema.

Yanga imemaliza mechi zake tatu maalum nchini Afrika Kusini, ikishinda mbili na kupoteza moja. Ilifungwa mabao 2-1 na FC Augsburg ya Ujerumani kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya TS Galaxy.

Leave a Comment