Kufuatia usajili wa Kylian Mbappe na Real Madrid katika dirisha la uhamisho la majira ya kiangazi kutoka PSG, swali kuu lililojitokeza ni nafasi gani atacheza. Sasa kocha wa timu hiyo, Carlo Ancelotti, ametoa majibu yake.
Kawaida, Mbappe anacheza zaidi kama winga wa kushoto, eneo ambalo katika kikosi cha Real Madrid limekaliwa na Vinicius Jr.
Akizungumza na The Obi One Podcast, Ancelotti alielezea: “Namuona Mbappe akicheza kama mshambuliaji wa kati, lakini ni muhimu zaidi kuwa na mchezaji anayejua kuhama maeneo.”
“Nikikuuliza Vinicius alicheza wapi msimu uliopita, ni vigumu kusema. Hakushikilia nafasi moja, wakati mwingine alicheza kushoto na wakati mwingine katikati.”
“Bellingham pia, kuna nyakati alicheza upande wa kushoto, katikati, na wakati mwingine kulia. Rodrygo alianza michezo mingi upande wa kulia lakini wakati mwingine alihama kwenda kushoto. Hili ni jambo muhimu.”
“Nataka kuwapa wachezaji wangu uhuru. Tulicheza dhidi ya Man City na Rodrygo na Vinicius walikuwa upande wa kushoto kwa sababu tuliona kuna kitu cha kipekee walichoweza kutoa kutoka eneo hilo.”
Pia Ancelotti aliulizwa jinsi atakavyomuingiza Mbappe kwenye timu, akasema: “Kuingia kwa Mbappe kwenye timu haitakuwa tatizo. Jambo muhimu ni yeye kuhakikisha anaendana na timu na kutoa mchango wake kwa asilimia kubwa.”
Mbappe hajajiunga na kikosi cha Real Madrid kilichoko Marekani kwa maandalizi ya msimu mpya baada ya kupewa mapumziko kutokana na jeraha la pua alilopata katika Euro 2024.