CAF Yapiga Faini MC Alger na Esperance kwa Vurugu za Mashabiki

0
CAF Yapiga Faini MC Alger na Esperance kwa Vurugu za Mashabiki

CAF Yaiadhibu Vikali MC Alger na Esperance kwa Vitendo vya Vurugu

Katika hatua ya hivi karibuni ya kusimamia nidhamu na utulivu katika mashindano ya kimataifa, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limezitoza faini klabu za MC Alger ya Algeria na Esperance ya Tunisia kutokana na vurugu zilizoibuka kwenye mechi zao za robo fainali ya mashindano ya CAF Champions League dhidi ya Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns.

Kamati ya nidhamu ya CAF ilibaini kuwa MC Alger ilihusika kwenye matukio ya fujo yaliyojitokeza Aprili 9 mwaka huu, wakati wa mchezo dhidi ya Orlando Pirates uliochezwa katika Uwanja wa Orlando jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Kutokana na tukio hilo, MC Alger imepigwa faini ya Dola 100,000 sawa na Shilingi milioni 269 za Tanzania.

Aidha, kocha msaidizi wa MC Alger, Mohamed Khezrouni, amefungiwa kutokea kwenye benchi katika mechi nne zijazo za CAF kutokana na kushiriki au kushindwa kudhibiti hali. Vilevile, beki wa timu hiyo Abdelkader Oussama Menezia amefungiwa mechi mbili.

Kwa upande wa Esperance, klabu hiyo ya Tunisia nayo imekumbwa na adhabu ya kiasi hicho hicho cha fedha, Dola 100,000, kwa vurugu za mashabiki wake zilizotokea Aprili 1 mwaka huu dhidi ya Mamelodi Sundowns katika Uwanja wa Loftus Versfeld, Afrika Kusini.

Katika mechi hiyo ya Aprili 1, Sundowns walifanikiwa kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Peter Shalulile. Ushindi huo wa ugenini uliwawezesha kusonga mbele kwa kuwa mechi ya marudiano iliyochezwa Tunisia ilimalizika kwa sare tasa (0-0).

Nayo Orlando Pirates ilifanikiwa kufuzu kwa hatua inayofuata baada ya kutoka sare ya bila kufungana nyumbani Aprili 9, huku ikiwa tayari imepata ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Aprili 1 dhidi ya MC Alger.

Hatua hizi za kinidhamu kutoka CAF ni ujumbe kwa vilabu vyote barani Afrika kuhakikisha wanazingatia nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya uwanja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here