Michezo

Boban Zirintusa Ajiunga na Tusker Kenya

Boban Zirintusa Ajiunga na Tusker Kenya

Timu ya Tusker ya Kenya imefanikiwa kumsajili mshambuliaji wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa, kwa mkataba wa mwaka mmoja.

Msimu uliopita, mchezaji huyo alionyesha kiwango cha juu katika timu ya Mara iliyo shiriki Ligi ya Championship baada ya kufunga mabao 21, sawa na mshambuliaji maarufu wa KenGold, Edgar William.

Akiongea na Mwanaspoti, Boban alisema kuwa licha ya kuwa na ofa nyingi, alichagua Tusker kutokana na kuvutiwa na timu hiyo. Alieleza kuwa kujiunga na Tusker ni hatua kubwa katika maisha yake kwani ni moja ya timu bora zaidi nchini Kenya.

“Ninajisikia kama nipo nyumbani Uganda kwa sababu mazingira hayana tofauti kubwa. Nashukuru kwa fursa niliyopata katika Ligi ya Championship msimu uliopita nikiwa na Biashara, kwani ndio iliyonifanya kufika hapa nilipo leo,” alisema.

Boban aliongeza kuwa moja ya mambo makubwa aliyoyakumbuka kuhusu soka la Tanzania ni ushindani mkubwa aliokutana nao. Mbali na Ligi Kuu Bara ambayo aliichezea, hata timu za madaraja ya chini zilikuwa na ushindani mkali.

Mchezaji huyo alijiunga na Biashara United akitokea Express FC ya Uganda na pia amewahi kucheza katika timu mbalimbali kama Mtibwa Sugar ya Tanzania, Polokwane City ya Afrika Kusini, Buildcon ya Zambia, Ethiopian Coffee ya Ethiopia, na Mohun Bagan AC ya India.

Boban ni miongoni mwa wachezaji wanaowania tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa mchezaji bora wa Ligi ya Championship zitakazofanyika Agosti Mosi, mwaka huu jijini Dar es Salaam, akiwa na Edgar William na Casto Mhagama wote wa KenGold.

Leave a Comment