Beno Kakolanya amejiunga na Namungo kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Ihefu, baada ya kuondoka Singida Fountain Gate ambako alicheza kwa miaka miwili. Kipa mpya wa Namungo FC, Beno Kakolanya, ameeleza matarajio yake ya msimu ujao kuwa ni kusaidia timu kumaliza katika nafasi nne za juu ili waweze kushiriki michuano ya kimataifa.
Kakolanya amesema, “Natarajia kuona tunamaliza katika nafasi itakayotuwezesha kushiriki michuano ya kimataifa, ambayo itatusaidia kuonyesha vipaji vyetu zaidi.”
Kakolanya anaamini kuwa na wachezaji wazoefu ndani ya kikosi cha Namungo ni kitu kinachompa matumaini makubwa ya mafanikio. Anataja wachezaji kama Meddie Kagere na Erasto Nyoni kuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia timu kupata ushindi wakati Ligi Kuu itakapoanza.
“Ndani ya timu kuna wachezaji wenye uwezo mkubwa na wazoefu kama Meddie Kagere, Erasto Nyoni, ambao nimewaona wakifanya vizuri katika mazoezi, na natarajia kuona matokeo chanya katika ligi,” amesema Kakolanya ambaye aliwahi kucheza Simba na Yanga ambazo mara kwa mara hushiriki michuano ya CAF.
Kakolanya amepongeza mapokezi mazuri aliyopata kutoka kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi, viongozi, na mashabiki wa Namungo, akiamini kuwa umoja huo utaleta mafanikio makubwa msimu ujao.
“Timu ikiwa na umoja ni silaha kubwa ya mafanikio. Naamini Namungo itafanya vizuri na kumaliza nafasi za juu msimu ujao,” amesema.