Michezo

Azim Dewji Atahadharisha Mashabiki wa Simba na Yanga

Azim Dewji Atahadharisha Mashabiki

Azim Dewji, mfadhili mkuu wa zamani wa Simba, amewataka wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga kuwa waangalifu wasiende mpirani na matokeo mfukoni. Dewji alisisitiza kuwa mechi za dabi hazitabiriki na mara nyingi timu bora hupoteza mechi hizo.

Azim Dewji Atahadharisha Mashabiki

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Dewji, ambaye aliifadhili Simba katika miaka ya 1990 na kuiwezesha kufanya vizuri kwenye michuano mbalimbali kama Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Kagame na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, alisema uzoefu wake unathibitisha kuwa matokeo ya dabi huamuliwa na dakika 90 za mchezo.

“Ni kweli ubora wa timu wakati mwingine huamua mechi, lakini mara nyingi tumeona Simba dhaifu ikiifunga Yanga bora na kinyume chake,” alisema Dewji. “Dabi haina mwenyewe, matokeo hutegemea uwezo wa wachezaji siku hiyo, jinsi walivyoamka na mbinu za walimu. Haiwezekani kusema kuwa Simba au Yanga watashinda kwa uhakika.”

Kesho, Simba na Yanga zitakutana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa mechi ya Ngao ya Jamii, kuashiria kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu. Dewji aliongeza kuwa timu zote zina wachezaji wazuri kama walivyoonyeshwa kwenye Simba Day na kilele cha Wiki ya Mwananchi. Hata hivyo, alionya kuwa Simba inahitaji muda zaidi kwa wachezaji wake wapya kuzoeana kabla ya kuwa timu ya kutisha.

“Simba ina wachezaji wapya 13, hivyo itachukua muda kabla ya kuanza kuonyesha ubora wao,” alisema Dewji.

Dewji pia alionyesha kutoridhishwa kwake na ukosefu wa wachezaji wengi wa Kitanzania kwenye timu hizo, akilinganisha na timu za Red Arrows ya Zambia na APR ya Rwanda ambazo zina wachezaji wengi wa kizawa.

“Red Arrows ilikuwa na asilimia 90 ya wachezaji wa Kizambia, tunahitaji kuelewa wapi tunakosea na kurekebisha hali hii,” alisema Dewji. Aliongeza kuwa kuondoa mpira shuleni ilikuwa kosa na ni vizuri kuwa sasa michezo imerudishwa shuleni.

“Nafikiri tulikosea kuondoa mpira shuleni, ndiyo sehemu kipaji cha mchezaji kinaanza kuonekana. Sasa michezo imerudishwa, tutegemee matokeo bora miaka michache ijayo,” alisema Dewji.

Leave a Comment