Ajira Tanzania

Aliyemuua Mkewe na Kukamatwa Baada ya Miaka 8, Apoteza Rufaa

Aliyemuua Mkewe na Kukamatwa Baada ya Miaka 8, Apoteza Rufaa

Mauaji ya Mkewe Yamupeleka Kunyongwa, Mahakama Yatupilia Mbali Rufaa

Mahakama ya Rufani nchini imethibitisha adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa Nyamhanga Joseph, mkazi wa Kiongera, Tarime, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Rhobi Nyamhanga.

Kwa mujibu wa mashitaka, tukio hilo lilitokea Juni 9, 2008, ambapo Nyamhanga alimpiga mkewe kwa fimbo huku akiwa na panga, akimzuia yeyote kuingilia ugomvi huo. Baada ya muda mfupi, marehemu alipatikana akiwa hajitambui karibu na Mto Kamachage na kufariki dunia alipofikishwa hospitalini.

Nyamhanga alikimbia mara baada ya tukio hilo na kufanikiwa kujificha kwa miaka minane kabla ya kukamatwa Februari 15, 2016, mkoani Mwanza.

Hukumu ya Awali na Rufaa

Baada ya kusikilizwa kwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tarime, Nyamhanga alitiwa hatiani na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa. Hata hivyo, hakuridhika na adhabu hiyo na hivyo kukata rufaa Mahakama ya Rufani, akidai ushahidi wa upande wa utetezi haukupewa uzito unaostahili.

Majaji wa Mahakama ya Rufani—Barke Sehel, Lucia Kairo, na Amour Khamis—walibaini kuwa upande wa mashitaka ulithibitisha kosa pasipo kuacha shaka yoyote. Mahakama ilizingatia kuwa mshtakiwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu akiwa na panga mkononi, na kutoroka kwake baada ya tukio kulionyesha hatia yake.

Jaji Sehel alisema:
“Mrufani alijitetea, lakini utetezi wake haukutilia shaka ushahidi wa mashitaka. Tumethibitisha kuwa ndiye aliyemkata marehemu shingoni na kusababisha kifo chake.”

Kwa mantiki hiyo, rufaa ya Nyamhanga ilitupiliwa mbali, na hukumu ya kunyongwa hadi kufa kusalia kuwa mwisho wa safari yake ya kisheria.

Ushahidi wa Mashahidi

Mashahidi wanne walitoa ushahidi mahakamani, akiwemo jirani wa wanandoa hao, Kasanya Magabe. Alieleza kuwa alimuona Nyamhanga akimpiga marehemu kwa fimbo huku akimzuia yeyote kuingilia kati kwa panga. Marehemu alipiga kelele akiomba msaada, lakini hakuna aliyethubutu kuingilia kati.

Baada ya dakika 25, shahidi huyo alipomfuata tena, alimkuta marehemu amelala hana fahamu karibu na mto, huku Nyamhanga na watoto wao wawili wakiendelea na safari yao kuelekea nyumbani.

Mama wa mshtakiwa, Meng’anyi Chango, aliripoti tukio hilo kwa mwenyekiti wa kijiji, na mwili wa marehemu ulipokaguliwa, ulikutwa na majeraha makubwa, yakiwemo jeraha lililosababisha shingo yake kuning’inia.

Daktari aliyefanya uchunguzi alithibitisha kuwa marehemu alifariki kutokana na kupoteza damu nyingi baada ya kupigwa na kitu butu.

Nyamhanga Akana Mashtaka

Katika utetezi wake, Nyamhanga alidai hakuwepo eneo la tukio siku hiyo na kwamba alirudi kijijini kwa ajili ya mazishi ya mkewe Mei 6, 2008, kabla ya kurejea Dar es Salaam.

Hata hivyo, ushahidi uliotolewa dhidi yake ulithibitisha kuwa alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na marehemu kabla ya kifo chake. Hatimaye, Mahakama ilithibitisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa, ikiashiria mwisho wa kesi hii ya mauaji.

Leave a Comment