Michezo

Ahmed Ally Amkataa Dulla Makabila: Hana Nafasi Simba Day

Ahmed Ally Amkataa Dulla Makabila

Ahmed Ally Amkataa Dulla Makabila

Msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, amezungumzia sakata lililozuka kuhusu msanii wa muziki wa Singeli, Dulla Makabila, kutumbuiza katika Tamasha la Simba Day.

Ahmed Ally amesema mashabiki wa Simba watulie kwani klabu hiyo haijamtangaza Dulla kutumbuiza siku hiyo. Hata kama angekuwa kwenye orodha, hatapewa nafasi hiyo kwa sababu tamasha hilo ni kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki, na kama hawamtaki, hawatamuweka.

Amesema hadi sasa msanii pekee aliyetangazwa kutumbuiza siku hiyo ni Alikiba pamoja na wengine waliotangazwa rasmi. “Tamasha hili ni kwa ajili ya burudani ya mashabiki wa Simba. Kama hawamtaki msanii, kwa nini tumuweke? Hatupo hapa kuwaudhi mashabiki wetu, na klabu haijamtangaza Dulla Makabila kama atatumbuiza siku hiyo. Umeiona taarifa hii kwenye akaunti rasmi ya Simba?”

Ahmed Ally aliongeza kuwa Simba imewatangaza wasanii watakaotumbuiza wakiongozwa na Alikiba, na habari kuhusu Dulla Makabila ni uvumi tu unaosambaa mitandaoni. “Hata kama angewekwa kwenye orodha, hatatumbuiza. Tunawaheshimu na kuwathamini mashabiki wetu, hivyo watulie tu,” alisema Ahmed Ally.

Kauli za Ahmed Ally zimekuja baada ya picha za wasanii watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo kusambaa mitandaoni, zikimjumuisha Dulla Makabila, na kusababisha baadhi ya mashabiki kumpinga vikali kutokana na kauli zake dhidi ya klabu hiyo.

Baada ya kuona maoni ya mashabiki, Dulla Makabila alijibu kupitia ukurasa wake wa Instagram, akisema yupo njiani kuelekea studio kuandaa wimbo ambao utawafanya mashabiki wa Simba wamtake na kumkubali. Dulla Makabila amekuwa akihama kati ya timu za Kariakoo, mara ya mwisho akitokea Simba na kurudi Yanga, na kabla ya hapo akitokea Yanga kwenda Simba.

Leave a Comment