Michezo

Ahmed Ally Afafanua Utata wa Jezi ya Manula

Ahmed Ally Afafanua Utata wa Jezi ya Manula

Uongozi wa Simba kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano umetolea ufafanuzi kuhusu jezi namba 28, ambayo imekuwa ikivaliwa na kipa Aishi Manula kwa misimu saba sasa. Juzi, wakati wa mechi dhidi ya Yanga, kipa mpya Moussa Camara, aliyesajiliwa kutoka AC Horoya ya Guinea, alionekana uwanjani akiwa na jezi namba 26 badala ya 28 iliyotajwa awali katika orodha ya kikosi.

Utata wa Jezi ya Manula

Kipa Manula, ambaye ana mgogoro na klabu, hakushiriki katika maandalizi ya msimu mpya nchini Misri, na alikosekana pia kwenye Tamasha la Simba Day. Hata hivyo, uongozi wa Simba ulifafanua kuwa Manula bado ni mchezaji wao, na tukio la kutojumuishwa kwake lilikuwa ni makosa ya bahati mbaya.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alieleza kuwa kosa lilitokea kwenye uandikwaji wa namba ya jezi ya Camara, na alithibitisha kuwa kipa huyo mpya atatumia jezi namba 26. Alisisitiza kuwa utata huo sasa umefutika, na Camara anajulikana rasmi kuwa ndiye mtumiaji wa jezi hiyo.

Simba imemsajili Camara ili kujaza nafasi ya Ayoub Lakred aliyeumia akiwa kambini Misri. Licha ya Camara kuruhusu bao moja katika mechi dhidi ya Yanga, alionyesha kiwango kizuri, na kuwafurahisha mashabiki wa Simba. Yanga walishinda mechi hiyo kwa bao 1-0 na watachuana na Azam FC kwenye fainali ya Ngao ya Jamii, huku Simba ikipambana na Coastal Union kusaka mshindi wa tatu.

Leave a Comment