Ruben Amorim Asisitiza Haondoki kwa Hiari
Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, ametamka kwa uwazi kuwa hatotangaza kujiuzulu licha ya matokeo mabaya yanayoikumba timu yake. Amorim amesema yuko tayari kuondoka klabuni endapo bodi ya Manchester United au mashabiki wataona kuwa hastahili kuendelea kuiongoza timu hiyo — lakini hawezi kuacha kazi kwa hiari yake mwenyewe.
Matokeo Mabaya Yalioibua Mjadala
Kauli hiyo ya Amorim imekuja mara baada ya Manchester United kupoteza fainali ya Europa League kwa bao 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspur. Matokeo hayo yameifanya United ikose nafasi ya kushiriki michuano yoyote ya Ulaya msimu ujao.
Tangu achukue mikoba ya ukocha mwezi Novemba mwaka jana, Manchester United imeshinda mechi 16 tu kati ya 41 na kwa sasa inashika nafasi ya 16 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England — hali ambayo imezua maswali kuhusu ufanisi wake.
Amorim: “Sitaondoka Kwa Hiari”
Katika mahojiano na waandishi wa habari, Amorim alinukuliwa akisema:
“Kama bodi au mashabiki wataona sifai, nitaondoka siku hiyo hiyo bila kudai fidia. Lakini mimi mwenyewe sitaacha kazi. Nina imani na ninachofanya.”
“Sita badilika katika mbinu zangu… najua najitahidi na ninahitaji muda kuleta mabadiliko.”
Anahitaji Imani na Muda
Amorim amekiri kuwa hali ndani ya Manchester United si shwari na kuna haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika kipindi cha dirisha la usajili la majira ya joto. Amewataka mashabiki kuwa na subira na imani huku akiendelea na kazi ya kujenga kikosi bora kitakachoweza kushindana katika viwango vya juu.
Mkataba Wake Bado Unaendelea
Licha ya kuwa na mkataba unaomfunga hadi mwaka 2027, Amorim hajifichi kuhusu uwezekano wa kutimuliwa ikiwa hali itaendelea kuwa mbaya. Hata hivyo, anaendelea kusisitiza kuwa bado ana maono ya kuirejesha Manchester United kwenye ubora wake wa kihistoria.
“Naendelea kupambana. Lengo langu ni kuhakikisha United inakuwa timu ya ushindani tena.”
Leave a Comment