Xabi Alonso Athibitisha Kuondoka Bayer Leverkusen
Kocha mkuu wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso, ametangaza rasmi kuwa ataondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu wa Bundesliga 2024/2025, akifunga ukurasa wa mafanikio baada ya takribani miaka mitatu ya kuiongoza timu hiyo ya Ujerumani.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Alonso alisema muda umefika kwa yeye kuhitimisha ukurasa wake na Leverkusen, ingawa hakuweka wazi anapopanga kwenda baada ya kuondoka. Akiwa na historia kama mchezaji katika klabu kubwa kama Real Madrid, Liverpool na Bayern Munich, Alonso amefanikiwa pia kama kocha kwa muda mfupi akiwa Leverkusen.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za michezo Ulaya, Alonso anaripotiwa kuwa tayari amekubaliana kujiunga na Real Madrid kwa mkataba wa miaka mitatu, akitarajiwa kuchukua nafasi ya Carlo Ancelotti ambaye anaelekea kuwa kocha wa timu ya taifa ya Brazil.
Xabi Alonso ameiwezesha Leverkusen kuwa moja ya timu tishio katika Bundesliga na mashindano ya kimataifa, akibadilisha kabisa taswira ya klabu hiyo. Msimu huu, Leverkusen imeonyesha ubora wa hali ya juu, ikiweka presha kubwa kwa wapinzani kama Bayern Munich na Borussia Dortmund.
Licha ya mafanikio hayo, kuondoka kwa Alonso kunachukuliwa kama pigo kubwa kwa Leverkusen, lakini pia ni fursa mpya kwa kocha huyo chipukizi anayetazamwa kama mmoja wa vipaji vikubwa zaidi vya ukocha barani Ulaya.
Uongozi wa Bayer Leverkusen umeonyesha shukrani kwa mchango wa Alonso na kumtakia mafanikio mema katika hatua yake ijayo. Wakati mashabiki wakisubiri uthibitisho wa rasmi wa uhamisho wake, dunia ya soka inasubiri kuona hatua ya pili ya safari ya ukocha wa Xabi Alonso, inayosemekana kuelekea Real Madrid.
Unadhani Real Madrid ni chaguo sahihi kwa Xabi Alonso katika hatua hii ya kazi yake ya ukocha?