Papa Francis Afariki Dunia Vatican Akiwa na Miaka 88

0
Papa Francis Afariki Dunia
Papa Francis Afariki Dunia

Papa Francis Afariki Dunia Akiwa na Miaka 88 – Dunia Yamlilia

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, amefariki dunia leo Aprili 21, 2025, akiwa na umri wa miaka 88 katika makazi yake ya Casa Santa Marta, Vatican. Taarifa rasmi imetolewa na Mwadhama Kardinali Farrell saa chache baada ya tukio hilo, akisema kwa huzuni: “Ndugu wapendwa, kwa huzuni kubwa sina budi kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu Francisko.”

Kardinali huyo alieleza kuwa Papa alifariki saa 7:35 asubuhi kwa saa za Vatican. “Maisha yake yote yaliwekwa wakfu kwa huduma ya Bwana na Kanisa Lake. Alitufundisha kuishi maadili ya Injili kwa uaminifu, ujasiri na upendo wa ulimwengu wote, hasa kwa maskini zaidi na waliotengwa zaidi,” aliongeza.

Katika maneno ya mwisho ya heshima, Kardinali Farrell alisema: “Kwa shukrani nyingi sana kwa ajili ya kielelezo chake kama mfuasi wa kweli wa Bwana Yesu, tunaipongeza roho ya Papa Francisko kwa upendo wa huruma usio na kikomo wa Mungu Mmoja na wa Utatu.”

Muonekano wa Mwisho Hadharani

Kifo chake kimetokea chini ya saa 24 baada ya kuonekana hadharani katika Uwanja wa St Peter’s kwa ajili ya maadhimisho ya Jumapili ya Pasaka. Akiwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu, Papa alipunga mkono kwa waumini waliokuwa wakishangilia na kusema: “Ndugu wapendwa, Pasaka njema.” Hotuba yake ilisomwa na msaidizi huku yeye mwenyewe akiwa ametulia, akitazama kwa utulivu.

Baada ya baraka hiyo, msafara wake ulizunguka uwanja ambapo alisimama mara kwa mara kubariki watoto wachanga waliokuwa wakiletwa mbele yake. Huo ndio ulikuwa muonekano wake wa mwisho hadharani.

Afya Yake Kabla ya Kifo

Papa Francis alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiafya katika miezi ya mwisho ya maisha yake. Mnamo Februari 14, alilazwa katika hospitali ya Gemelli, Roma, kwa matibabu ya homa ya mapafu. Alikuwa akipata tabu kupumua kwa siku kadhaa. Aliruhusiwa kutoka hospitalini Machi 23, lakini hali yake iliendelea kudhoofika.

Historia yake ya kiafya ilihusisha kuondolewa sehemu ya mapafu alipokuwa kijana, hali iliyomfanya kuwa hatarini zaidi kushambuliwa na homa ya mapafu, ugonjwa unaosababishwa na bakteria, virusi au fangasi.

Dunia Yamlilia Papa Francis

Viongozi kutoka pande mbalimbali za dunia wametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu. Ikulu ya White House ilichapisha ujumbe kwenye mtandao wa X ukisema: “Pumzika kwa Amani, Papa Francis” sambamba na picha ya Papa akiwa na Rais Donald Trump na Melania, pamoja na picha nyingine ya mkutano wake na JD Vance.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, alimtaja Papa kama “kiongozi wa mamilioni, hata nje ya Kanisa Katoliki, aliyesimama kwa unyenyekevu na upendo safi kwa wasiojiweza.” Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, alisema “ameumizwa sana” na taarifa za kifo hicho. Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Poland, Donald Tusk, alimkumbuka Papa kama “mtu mzuri na mchangamfu.” Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, alimwelezea kama “sauti ya amani, upendo na huruma.”

Kwa sasa, maandalizi ya mazishi yanaendelea Vatican huku ulimwengu ukitafakari maisha ya huduma, upendo na utumishi ya Baba Mtakatifu Francis.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here