Taasisi za Serikali Kwenye Ulingo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Leo
Mechi kali za Ligi Kuu Tanzania Bara zinaendelea leo Ijumaa, Aprili 18, 2025, ambapo timu nne zinazomilikiwa na taasisi za kiserikali zitashuka dimbani katika viwanja viwili tofauti.
Michezo hiyo miwili itaanza saa 10:00 jioni na inahusisha timu kutoka taasisi za ulinzi na usalama pamoja na zile za serikali za mitaa.
Katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, kutakuwa na pambano kati ya Tanzania Prisons dhidi ya JKT Tanzania. Hii ni mechi yenye uzito mkubwa kwa Tanzania Prisons ambayo bado inahaha kusalia kwenye ligi, ikiwa na pointi 24 na kushika nafasi ya 14 katika msimamo. Kwa upande mwingine, JKT Tanzania yenye pointi 32 ipo nafasi ya saba na tayari imejihakikishia kubaki ligi kuu msimu ujao.
Mechi ya pili itapigwa katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam kati ya KMC na Dodoma Jiji. Huu ni mchuano wa timu mbili chini ya Wizara ya TAMISEMI. KMC inahitaji ushindi zaidi ili ijinasue kwenye hatari ya kushuka daraja, ikiwa nafasi ya 13 na pointi 27. Dodoma Jiji wao wapo kwenye nafasi salama wakiwa na pointi 34.
Kocha msaidizi wa KMC, Steve Nyenge ameeleza kuwa wamejipanga vyema kwa ajili ya mchezo huo na wanaingia kwa tahadhari kutokana na ubora wa wapinzani wao. “Tunaujua uzuri wa timu ya Dodoma Jiji na udhaifu wao. Lazima twende kwa tahadhari hivyo tutajilinda na kushambulia ili tuhakikishe tunapata matokeo mazuri,” alisema.
Kwa upande wa Dodoma Jiji, kocha Mecky Maxime amesema kuwa kila mechi iliyobaki ni fainali kwao na wanahitaji pointi tatu muhimu kwenye kila mchezo.
Matarajio ya mashabiki ni kuona mechi zenye ushindani na nidhamu ya hali ya juu huku kila timu ikisaka alama muhimu kwa malengo tofauti, wengine wakisaka kupona na wengine kutafuta nafasi bora zaidi msimu ukielekea ukingoni.