Makudubela Anang’ara Congo, Yanga Waliacha Ligi Kubwa Kupita
Habari kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Kinshasa) zinadai kuwa Skudu Makudubela, aliyewahi kuwa mchezaji wa Klabu ya Yanga SC, kwa sasa anaonyesha kiwango cha juu sana ambacho hakukionyesha alipokuwa Tanzania. Mchezaji huyo ambaye alionekana kufeli Ligi Kuu ya Tanzania sasa ni tishio kubwa kwenye ligi ya Congo, kiasi kwamba mabeki wa timu pinzani wanamwogopa.
Takwimu zinaonyesha kuwa Makudubela amefunga mabao kumi (10) na kutoa pasi za mwisho nne (4) katika mechi sita (6) alizocheza tangu aanze msimu huu. Hii ni dalili kuwa kuna changamoto fulani ambazo wachezaji wa kigeni wanapitia wanapowasili Tanzania, changamoto ambazo mara nyingi haziwekwa wazi kwa umma.
Mfano mwingine ulio hai ni ule wa mshambuliaji Fiston Mayele, aliyekuwa na kipindi kigumu cha kufunga mabao akiwa Yanga. Ilifikia hatua ambapo ilibidi atafute msaada wa kiroho na kwenda kuombewa na Mwamposa, hatua ambayo ilibadilisha kabisa hali yake uwanjani. Baada ya maombi hayo, Mayele alianza kufumania nyavu mara kwa mara, hali iliyomvutia hadi kusajiliwa na klabu ya Pyramids ya Misri. Alipopata mafanikio, alirudi Tanzania kumshukuru Mwamposa na kumkabidhi jezi yake kama ishara ya kuthamini msaada wake.
Mwenendo huo haukumalizikia kwa Mayele pekee. Wachezaji wengine waliopitia hali kama hiyo ni Prince Dube na Lionel Ateba, ambao walipoombewa, walibadilika ghafla na kuanza kufunga mabao huku wakikosa nafasi za wazi mara chache sana. Matokeo yao yakawa mazuri kuliko ilivyotarajiwa awali.
Hali hii imeibua maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka, hasa kuhusu nini hasa kinachowasibu wachezaji wa kigeni wanapowasili Tanzania, na ni kwanini baadhi yao hushindwa kuonesha uwezo wao halisi. Je, ni mazingira ya ligi? Ni presha kutoka kwa mashabiki? Au kuna mambo ya kiimani yanayohusika?
Katika mazingira ya soka la kisasa, ambapo mafanikio yanategemea zaidi ya mazoezi na vipaji, inaonekana dhahiri kwamba baadhi ya wachezaji wanatafuta msaada wa ziada kuhakikisha wanang’ara – iwe ni maombi au mbinu nyingine zisizo za kawaida.
Kwa sasa, Makudubela anaendelea kung’ara na kuonyesha kuwa bado ana uwezo mkubwa, na hilo linaacha maswali kwa uongozi wa zamani wa Yanga SC waliomtoa – je, walimwelewa kweli au walihukumu mapema?